Alhadj Dk.Hussein Ali Mwinyi,ameitaka Kamati ya Msikiti wa Masjid Taqwa kushirikiana na waumini wa mskiti huo katika utatuzi wa changamoto mbali mbali zinazoikabili jamii.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhadj Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameitaka Kamati ya Msikiti wa Masjid Taqwa kushirikiana na waumin wa mskiti huo katika utatuzi wa changamoto mbali mbali zinazoikabili jamii.Alhadj Dk.Mwinyi ametowa wito huo leo katika Ufunguzi wa msikiti mkuu wa Ijumaa wa ‘Masjid Taqwa’ uliopo Bambi Wilaya ya Kati,Mkoa Kusini Unguja,uliojengwa kwa mashirikiano kati ya wananchi na Mfadhili.

Amewataka waumini hao kuutumia msikiti huo kama kituo cha kujifunza na kuzungumzia matatizo yanayoikabili jamii, kama vile changamoto za maisha zinazowahusu mayatima, wajane pamoja na vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto.Alisema mbali na Ibada ya swala, pia kuna umuhimu wa kuendeleza na kuutumia msikiti huo katika mambo mbali mbali, kwa mujibu wa mafunzo ya Mtume Muhammad (SAW).

Alhadj Dk. Mwinyi alisiitiza umuhimu wa waumini wa msikiti huo kuutunza ili uweze kudumu kwa miaka mingi ijayo.Aidha, aliwaeleza waumini wa msikiti huo wajibu walionao katika kufanya mambo mema ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya akhera yao, akibainisha kila muumini ana nafasi ya kuimarisha msikiti huo katika matunzo, ikiwemo kusaidia huduma za maji, umeme au kuufanyia matengenezo madogo madogo.

Katika hatua nyengine, Alhadj Dk. Mwinyi alipongeza juhudi za waumini wa kijiji hicho kwa kuunganisha nguvu zao na kuanza kazi ya ujenzi wa msikiti huo mkubwa badala ya kusubiri mfadhili.Aidha, aliwataka waumini kuwangalia kwa njia ya kuwasaidia waumini wanaojitolea kusaidia maendeleeo ya dini,  wakiwemo maimamu na walimu, akibainisha wanakabiliwa na maisha duni.

Rais Alhadj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuahidi kuzifanyia kazi changamoto za mawasiliano ya simu na barabara ambazo zimekuwa kikwazo kwa wananchi wa kijiji cha Bambi, ambapo pamoja na mambo mengine huzorotesha hughuli zao za kiuchumi.

Mapema, Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Rashid Hadidi, alitoa shukurani kwa Rais Alhadj Dk. Mwinyi kwa kujumuika pamoja na waumin wa Msikiti huo katika hafla hiyo muhimu ya ufunguzi wa msikiti, sambamba na kuishukuru Kamati ya Msikiti na Msimamizi wa ujenzi kwa kukamilisha kazi hiyo kwa ufanisi.

Nae, Naibu Kadhi wa Zanzibar, Sheikh Othman Hassan Ngwali aliwataka waumini wa msikiti huo kuuimarisha kwa njia mbali mbali, ikiwemo ya kutumika kwa shughuli za kujifunza.Aidha, akisoma Risala ya waumini wa msikiti huo, Sheikh Omar Abdalla, alisema ujenzi wa msikiti huo wenye uwezo wa kuswaliwa na waumini wapatao 2000,  umetokana na ajali ya kuungua moto kwa msikiti wa mwanzo miaka minne iliyopita.

Alisema ujenzi wa msikiti huo mpya umefanyika kutokana na michango ya waumini mbali mbali, ikiwemo wa kutoka kijiji hicho, Zanzibar na nje ya Zanzibar pamoja na mfadhili.Sheikh Omar kwa niaba ya Kamati ya Msikiti huo alitoa shukurani   kwa waumini wote waliosaidia na kufanikisha ujenzi wa msikiti huo pamoja na kutoa ahadi ya kuutunza na kutumika kwa misingi iliyokusudiwa.

Alimuomba Rais wa Zanzibar kuzitafutia ufumbuzi changamoto za mawasiliano yasioridhisha ndani ya kijiji hicho pamoja na ubovu wa barabara itokayo kijiji hicho hadi Pongwe Pwani kwa kigezo kuwa imekuwa kikwazo katika shughuli za kiuchumi.

Viongozi mbali mbali wa Kitaifa walishiriki katika hafla hiyo, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Mstaafu Balozi Seif Ali iddi ,Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, masheikh pamoja na waumini kutoka maeneo mbali mbali ya Kisiwa cha Unguja.