Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Zanzibar imetakiwa kushirikiana vyema na Chama cha SKAUTI Tanzania.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza haja kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Zanzibar kushirikiana vyema na Chama cha SKAUTI Tanzania ili kuwajengea vijana uwezo mzuri wa stadi za maisha pamoja na uzalendo.Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo, Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na Uongozi wa Chama cha SKAUTI Tanzania ukiongozwa na kiongozi wake Mkuu Hajjat Mwantumu Bakari Mahiza akiwa amefuatana na viongozi kutoka Zanzibar.

Alisema kuwa kuna vijana wengi wa SKAUTI waliohamasika katika chama hicho hapa Zanzibar hivyo, ni vyema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ikashirikiana na chama hicho katika kuhakikisha vijana hao wanatekelezewa mahitaji yao kutokana na shughuli wanazozifanya.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa programu za vijana ambazo tayari zimeshafanyika kwa upande wa Tanzania Bara ni nzuri na zinahitajika hasa kwa vijana na kueleza kwamba kuna vijana wengi wamehamasika kujiunga na chama hicho hivyo, ni vyema wakatumiwa vizuri ili lisijekuwa jeshi la kufanya mambo mabaya hapo baadae.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba programu hizo zifanywe japo kwa awamu kutokana na uwezo uliopo wa kifedha kwa Wizara ya Elimu ili vijana waweze kupata mafunzo hayo ambayo yatawasaidia katika stadi zao wa maisha.

Rais Dk. Mwinyi pia, alitoa maelekezo ya kurejeshewa kwa ofisi zake zilizokuwa zikitumiwa na chama hicho hapa Zanzibar ili chama hicho kiweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ni vyema kwa Wizara ya Elimu kutafuta njia ya kukutana na vijana hao wa SKAUTI huku akieleza haja ya Wizara hiyo kuwawezesha vijana wa SKAUTI kufanya programu hizo.

Rais Dk. Mwinyi pia, alipokea pongezi za ushindi wake uliomuwezesha kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kutoka kwa uongozi huo wa SKAUTI.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Khamis Juma amesema kuwa tayari Wizara yake imetenga fungu maalum kwa ajili ya SKAUTI, hivyo aliahidi Wizara hiyo kuwa itaendelea kutoa ushirikiano wake kwa chama hicho.

Mapema Mkuu wa Chama cha SKAUTI Tanzania Mwantumu Bakari Mahiza alitoa maombi ya chama cha SKAUTI Tanzania kwa upande wa Zanzibar na kueleza kwamba chama hicho kimekuwa kikiwashirikisha vijana kuanzia miaka 5 hadi 26 ambapo huwajenga kuwa weledi,  wazalendo, kuwapa makuzi bora na kuwa waadilifu.

Hivyo, katika maelezo yake Mkuu huyo alisema kuwa tayari kwa upande wa Tanzania Bara SKAUTI wameshafanyiwa mafunzo mbali mbali ya kuwajengea uwezo vijana hao ambayo ni vyema na vijana wa SKAUTI wa Zanzibar nao wakayapata.

Alieleza kuwa kutokana na kuwepo kwa tatizo sugu la rushwa nchini aliiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutoa baraka zake kwa vijana wa SKAUTI wa Zanzibar kupewa mafunzo ya rushwa ili wajue kwamba rushwa inaathari kubwa katika jamii.

Aidha, alisema kuwa programu nyengine ni ile ya uokoaji ikiwemo kuzuia moto katika maeneo ya skuli, kwenye makaazi na uokoaji katika mito, bahari na sehemu nyenginezo ambapo aliona haja kwa vijana wa SKAUTI wa Zanzibar kupata mafunzo kama hayo ambayo yatawasaidia kujua visababishi vya moto na vipi watajikinga kwa hatua za awali.

Alisema kuwa kwa upande wa Zanzibar SKAUTI ina miaka 109 na vijana waliopita wamepata mafunzo mbali mbali yakiwemo kutoa taarifa kwa Serikali hivyo, ni vyema kwa vijana wa Zanzibar nao kupata mafunzo hayo kwani tayari programu za kuwajengea uwezo katika skuli zimetolewa kwa walimu wa Tanzania Bara ambapo tayari zimeshafanyika kwa mikoa 14 na tayari mikoa 12 ya Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati na Magharibi mafunzo hayo yameshafanyika.

Hivyo, Mkuu huyo wa SKAUTI Tanzania alieleza haja kwa vijana wa Zanzibar nao wakapata mafunzo hayo ili kuwawezesha   kutoa taarifa na kusisitiza kwamba kizazi cha sasa kina hitaji kulelewa vyema ikiwa ni pamoja na kuwa na maadili mazuri.

Pia, kiongozi huyo alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa ushindi wake wa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi huku akieleza haja ya kurejeshewa ofisi yao ya SKAUTI ya hapa Zanzibar waliyokuwa wakitumia hapo siku za nyuma katika jengo lililokuwa la ofisi za ‘American Conner’ ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi.